Moja ya changamoto kubwa kwa watu wanaoanza kutumia website ni kuweka domain halafu website isifunguke. Unaweza kuwa umenunua domain, umeweka hosting, ume-upload website, lakini ukiandika jina la domain kwenye browser unaona error, ukurasa mweupe, “site can’t be reached,” “not secure,” au website ya zamani bado inaonekana. Hali hii inaweza kuchanganya, lakini mara nyingi huwa inasababishwa na vitu vichache vinavyoweza kutatuliwa.
Sababu ya kwanza ni DNS propagation. Unapobadilisha nameserver au DNS records za domain, mabadiliko hayo hayafanyi kazi dunia nzima kwa sekunde moja. Mitandao mbalimbali inahitaji muda kusoma mabadiliko mapya. Hii inaweza kuchukua dakika chache, masaa kadhaa, au wakati mwingine hadi saa 24 au zaidi kulingana na provider na mtandao unaotumia.
Kwa mfano, unaweza kuweka nameserver mpya leo, halafu kwenye simu yako website bado haifunguki, lakini kwenye computer ya mtu mwingine inafunguka. Hii inaweza kuwa ni kwa sababu mtandao mmoja umeshapata DNS mpya na mwingine bado una cache ya zamani. Hapo si lazima website iwe imeharibika; inaweza kuwa bado DNS haijasambaa kikamilifu.
Sababu ya pili ni nameserver kuandikwa vibaya. Hosting provider wako akikupa nameserver kama ns1.examplehost.com na ns2.examplehost.com, lazima uziandike kwa usahihi kwenye sehemu ya domain management. Ukikosea herufi moja tu, domain inaweza kushindwa kuelekezwa kwenye hosting sahihi.
Ni muhimu ku-copy nameserver moja kwa moja kutoka kwa hosting provider na ku-paste kwenye domain provider wako. Epuka kuandika kwa mkono kama huna uhakika, kwa sababu kosa dogo linaweza kusababisha website isifunguke kabisa.
Sababu ya tatu ni domain kutoelekezwa kwenye server sahihi. Wakati mwingine unaweza kutumia A record badala ya nameserver. A record inaelekeza domain kwenye IP address ya server. Kama IP ulioweka si sahihi, browser itajaribu kufungua server isiyo na website yako. Matokeo yake unaweza kuona error au website nyingine.
Kama hosting yako imekupa IP address, hakikisha A record ya domain yako inaelekeza kwenye IP hiyo. Pia kama unatumia www, hakikisha www nayo imeelekezwa vizuri kupitia CNAME au A record kulingana na maelekezo ya hosting yako.
Sababu ya nne ni SSL kutokuwekwa au kutokamilika. SSL ndiyo inafanya website ifunguke kwa https. Kama SSL haijawashwa vizuri, website inaweza kuonyesha ujumbe kama “Not Secure,” “Your connection is not private,” au browser ikazuia kufungua website.
Baada ya kuunganisha domain na hosting, hakikisha SSL certificate imewashwa. Hosting nyingi zina Let’s Encrypt SSL ya bure, lakini wakati mwingine unatakiwa kuibofya mwenyewe kwenye control panel. Kama domain bado haijaelekezwa vizuri, SSL pia inaweza kushindwa kutolewa kwa sababu system haiwezi kuthibitisha domain.
Sababu ya tano ni website files kuwekwa sehemu isiyo sahihi. Kwenye hosting, mara nyingi kuna folder maalum la kuweka website kama public_html, htdocs, www, au folder lenye jina la domain. Uki-upload mafaili sehemu tofauti, domain inaweza kufunguka lakini isione website yako.
Kwa mfano, kama hosting inahitaji mafaili ya website yawe ndani ya public_html, lakini wewe umeweka ndani ya folder nyingine, browser inaweza kuonyesha “index of,” “403 forbidden,” au ukurasa tupu. Hakikisha homepage yako kama index.html, index.php, au system yako ipo kwenye folder sahihi.
Sababu ya sita ni homepage file kukosekana. Website nyingi za kawaida zinahitaji file la mwanzo kama index.html au index.php. Kama file hili halipo, server inaweza kushindwa kujua ukurasa gani uonyeshwe kwanza. Hii inaweza kusababisha kuona list ya files au error.
Kama unatumia WordPress, hakikisha files zake zote zimewekwa vizuri na database imeunganishwa. Kama unatumia website ya HTML, hakikisha index.html ipo kwenye root folder ya website. Kama unatumia Django au framework nyingine, hakikisha server ime-configured kupeleka request kwenye application yako.
Sababu ya saba ni database connection problem. Kama website yako inatumia database, website inaweza kushindwa kufunguka kama database name, username, password au host si sahihi. Hili hutokea sana kwenye WordPress, Laravel, Django au systems zinazotumia database.
Kwa WordPress, unaweza kuona ujumbe kama “Error establishing a database connection.” Kwa Django au Laravel, unaweza kuona error ya database au ukurasa mweupe kulingana na settings. Hakikisha database imeundwa, user amepewa ruhusa, na credentials zimeandikwa vizuri kwenye configuration file.
Sababu ya nane ni settings za application kuwa bado zinaonyesha domain ya zamani. Kama umehamisha website kutoka domain moja kwenda nyingine, system inaweza kuwa bado inatumia domain ya zamani kwenye settings. Hii inaweza kusababisha redirect kwenda domain ya zamani au links kushindwa kufanya kazi.
Kwa WordPress, angalia Site URL na Home URL. Kwa Django, angalia ALLOWED_HOSTS, CSRF trusted origins, static files na media settings. Kwa Laravel, angalia APP_URL kwenye .env. Kila system ina sehemu zake za kuweka domain sahihi.
Sababu ya tisa ni ALLOWED_HOSTS kwenye Django kutowekwa vizuri. Kama unatumia Django na domain yako haipo kwenye ALLOWED_HOSTS, unaweza kupata error ya “DisallowedHost.” Hii ina maana Django imepokea request kutoka domain ambayo haijaruhusiwa kwenye settings.
Mfano, kama domain yako ni example.co.tz, kwenye settings unaweza kuhitaji kuweka:
ALLOWED_HOSTS = ["example.co.tz", "www.example.co.tz"]
Baada ya kubadilisha settings, mara nyingi unatakiwa ku-restart application au server ili mabadiliko yaanze kufanya kazi.
Sababu ya kumi ni static files kutopangwa vizuri. Hili linaweza kufanya website ifunguke lakini ionekane imeharibika, bila CSS, bila picha au bila mpangilio mzuri. Watu wengi husema “website imefunguka lakini design haionekani.” Mara nyingi hii ni static files problem.
Kwa WordPress, hii inaweza kutokana na URL za zamani au permissions. Kwa Django, hakikisha ume-run collectstatic, umeweka STATIC_URL, STATIC_ROOT, na server yako inaruhusu static files kufunguka. Pia hakikisha .htaccess, Nginx au Apache configuration haizuii static files.
Sababu ya kumi na moja ni cache ya browser au cache ya DNS. Wakati mwingine website imesharekebishwa lakini browser yako bado inaonyesha taarifa za zamani. Jaribu kufungua website kwa incognito mode, kufuta cache, kutumia browser nyingine, au kutumia network nyingine.
Unaweza pia kujaribu kufungua website kwa kutumia simu kupitia mobile data badala ya WiFi. Kama inafunguka kwenye mobile data lakini haifunguki kwenye WiFi, inawezekana mtandao wa WiFi bado una DNS cache ya zamani.
Sababu ya kumi na mbili ni hosting account kutokuwa active. Kama hosting haijalipiwa, ime-expire, au account imesimamishwa, website haitafunguka vizuri. Wakati mwingine utaona page ya hosting provider inayosema account suspended au domain parked. Hakikisha domain na hosting vyote vipo active.
Sababu ya kumi na tatu ni domain ku-expire. Kama domain imeisha muda wake na haijarenewiwa, website inaweza kuacha kufanya kazi hata kama hosting ipo sawa. Domain ikiexpire, mtu akiandika jina la website browser haiwezi tena kuielekeza vizuri kwenye hosting yako.
Ni vizuri kuweka reminder ya renewal ya domain na hosting kabla havijaisha. Website ikishuka kwa sababu domain ime-expire, inaweza kuathiri wateja, SEO na uaminifu wa biashara yako.
Sababu ya kumi na nne ni file permissions kuwa vibaya. Server inahitaji ruhusa sahihi kusoma mafaili ya website. Kama permissions zimekosewa, unaweza kupata error kama “403 Forbidden” au website kushindwa kusoma baadhi ya files. Kwa kawaida, folders na files zinapaswa kuwa na permissions zinazokubalika na hosting yako.
Sababu ya kumi na tano ni error kwenye code. Kama website ni ya custom code, kosa dogo kwenye settings, import, database query, template au dependency linaweza kufanya website isifunguke. Hili hutokea sana baada ya ku-upload version mpya ya website au kuhamisha project kwenda server mpya.
Kwa Django, unaweza kuangalia error logs za server ili kujua kosa ni nini. Kwa PHP au WordPress, unaweza kuwasha debugging kwa muda au kuangalia error log kwenye hosting panel. Usibaki kubahatisha; logs ndizo zinaonyesha chanzo halisi cha tatizo.
Ili kutatua tatizo la website kutofunguka, anza kwa kuangalia domain. Hakikisha domain haija-expire. Kisha angalia nameserver au DNS records. Baada ya hapo angalia kama hosting ipo active. Kisha hakikisha website files zipo kwenye folder sahihi. Baadaye angalia SSL, database, settings za application na error logs.
Kama website inafunguka bila www lakini haifunguki na www, tatizo linaweza kuwa kwenye DNS ya www. Kama inafunguka kwa http lakini haifunguki kwa https, tatizo linaweza kuwa SSL. Kama inafunguka lakini haina design, tatizo linaweza kuwa static files au CSS. Kama inaonyesha error ya database, tatizo liko kwenye database settings.
Ni muhimu kutenganisha tatizo badala ya kusema tu “website haifunguki.” Jiulize: haifunguki kabisa? Inaleta error gani? Inafunguka kwenye network nyingine? Inafunguka bila www? Inafunguka kwa http? Inaleta ukurasa mweupe? Inakosa CSS? Maswali haya yanasaidia kupata suluhisho haraka.
Kwa ujumla, website kutofunguka baada ya kuweka domain si lazima imaanishe website imeharibika. Mara nyingi tatizo huwa DNS, nameserver, SSL, folder, database, cache au settings ndogo za server. Ukifuata hatua kwa hatua, unaweza kugundua chanzo na kurekebisha.
Kumbuka: baada ya kubadilisha DNS au nameserver, kuwa na subira kidogo. Lakini kama masaa mengi yamepita na website bado haifunguki, angalia settings zako kwa makini au wasiliana na hosting provider/developer akusaidie kuangalia logs na configuration.